naQonda

CBC Grade 8 Kiswahili End Term 1 Exam 2025 · Question 11

b) Eleza ni vipi ukiukaji wa haki za watoto unaweza kuepukwa. (maneno 30-35) (alama 4, utiririko 1)

From Kiswahili — End Term One Assessment 2025 (Set 6) · 5 marks · Topic: Kusoma, Muhtasari

Soma taarifa ifuatayo kwa makini kisha ujibu maswali yanayofuata.
Nchi nyingi duniani zimetia saini mkataba wa umoja wa mataifa kuhusu haki za watoto.
Haki ni mambo mema ambayo watoto wanastahili kutendewa. Kwa kutia saini, nchi hizi zimetangaza kujitolea kwao kuzilinda na kuhakikisha kuwa hakuna ukiukaji wake na kuwa watoto wote katika himaya zao wananufaika kutokana na haki hizi.
Miongoni mwa haki hizi ni kuwa kila mtoto ana haki ya kuishi na kupata chakula cha kutosha na chenye viinilishe bora. Pili, kila mtoto ana haki ya kupata elimu. Elimu hii inafaa kutolewa bila ada na iwe inayofaa na inayopatikana kwa urahisi.Kisha kila mtoto ana haki ya kutopigwa na kutodunishwa kwa namna yoyote, iwe kitabaka, kirangi, kijinsia na vinginevyo. Mtoto ana haki pia kutolazimishwa kufanya kazi za kiutumwa, nzito na za kushurutishwa. Hali kadhalika, ana haki ya kuishi katika nyumba au makazi bora na salama, kutunzwa na kulindwa dhidi ya hali yoyote inayoweza kumhatarisha. Anatakiwa ashirikishwe katika kufanya maamuzi. Fauka ya haya, ana haki ya kupata huduma za afya,mahitaji maalum,michezo, upendo na habari. Isitoshe,anastahili kuheshimiwa kimawazo na kihisia. Haki hizi zinatakiwa kulindwa na kila mwanajamii, hivyo serikali za mataifa mengi zimeshirikisha haki hizi katika katiba za nchi zao na sheria zao.
Walakini haki hizi bado zinakiukwa. Watoto wengi kote duniani bado wananyimwa haki zao. La kusikitisha na kukera ni kuwa wanaotarajiwa kuwa vigogo vya kuzilinda haki hizi, ndio wanaoongoza kuzikiuka. Kila siku tunasikia na kushuhudia visa vya watoto kupigwa, kunyimwa chakula, kufanyishwa kazi kipunda, kuteswa, kuishi katika mazingira hatari, na hata kuuawa. Kuna watoto wengi wanaolala nje, wengine hawapati chakula licha ya kuwa wanatakiwa kupata chenye lishe bora. Kwao kutarajiwa mlo awamu tatu kwa siku ni njozi kwani hata awamu moja ni adimu kupata.
Watoto wengi katika mataifa yenye fujo na ghasia hutekwa na kutumikishwa vitani. Viongozi katika mataifa haya hawafanyi kitu ila kutazama tu wakati watoto wanaotakiwa kuwalinda wanageuzwa kuwa mibaba ya kuua na kuuana. Watoto hawa huvishwa magwanda ambayo miili yao minyonge haiwezi kuyahimili. Pia, huvalishwa mabuti ya kijeshi ambayo ni mizigo mizito ya kubeba mbali na bunduki zinazokaribia kuwazidi uzani wakati wanatakiwa kuwa wamelindwa majumbani, na shuleni na wazazi wao na serikali.
Jukwaa la vijiji vya mataifa ya ulimwengu wa tatu limesheheni watoto wasioenda shule kwa sababu ya lindi la ufukara uliokithiri. Elimu ya bure inayogusiwa katika haki za watoto haipo. Wanaong’ang’ana iwepo ni kana kwamba ni waota ndoto mchana. Jiulize watoto wangapi sasa hivi wamo majumbani bila kwenda shuleni kutokana na ukosefu wa karo? Wangapi wamo mitaani wakivuta na kunusa gundi huku wakiombaomba vishilingi?
Hali ilivyo sasa hivi inadai kuwa mimi na wewe tufanye hima na kuungana mikono kutafuta suluhisho la kudumu kuhusu haki za watoto. Twapasa kuhimiza serikali zetu kufanya kila ziwezavyo kuhakikisha kuwa watoto wote wamo shuleni. Nasi tushirikiane kutoa huduma kwa watoto na kukomesha dhuluma, mateso na dhiki kwao. Haitoshi kupeleka miswada mbungeni kuhusu haki za watoto na kuipitisha kuwa sheria. Twastahili kubadilisha misimamo yetu kuhusu haki hizi na kuzilinda kwa dhati bali si kwa chati.

b) Eleza ni vipi ukiukaji wa haki za watoto unaweza kuepukwa. (maneno 30-35) (alama 4, utiririko 1)

Answer

Tuungane kutafuta suluhisho la kudumu, tuhimize serikali kuhakikisha watoto wote wako shuleni, tushirikiane kuwahudumia watoto na kukomesha dhuluma na mateso dhidi yao, na tubadilishe misimamo yetu ili kuzilinda haki hizi kwa dhati.

Aya ya mwisho.

Written answers can be worded differently: naQonda marks your own answer and explains it when you sign up free.

Answer this test freeGet it marked: create a free account

More Grade 8 Kiswahili questions from this test