naQonda

CBC Grade 8 Kiswahili Exam Term 2 2026 · Question 9

Yafuatayo ni madhara ya vifaa vya kidijitali kwa mujibu wa kifungu isipokuwa

From Kiswahili — Term 2 Assessment May 2026 (Set 1) · 1 mark · Topic: Kusoma, Ufahamu wa Makala

Soma kifungu kifuatacho kisha ujibu swali la 1 mpaka la 10.

Babu alipofika katika kituo cha mabasi, alipiga simu akamfahamisha mama kuhusu kuwasili kwake. Mama alimwomba apumzike hapo kituoni kwa muda mfupi ili mimi na dada yangu tuende tukamlaki na kumbebea mkoba wake. Tuling’oa nanga na kutembea chapuchapu hadi kituoni. Baada ya kujuliana hali, niliupokea mzigo alikuwa nao, naye dada akambebea mkoba wake. Tulipiga gumzo tukielekea nyumbani. Likizo hiyo, aliamua kututembelea yeye mwenyewe kinyume na ilivyokuwa hapo awali.

Chambilecho wahenga, mgeni njoo mwenyeji apone. Kuja kwa babu kulileta furaha mzomzo pale nyumbani. Alikuwa ameandaliwa sima, mboga za kiasili na kitoweo cha kuku. Aidha, alipikiwa chai nzito ya maziwa iliyotiwa sukari kiasi. Tulikaa pamoja tukashtaki njaa kisha tukaanza kupiga soga. Babu alitujulisha kuwa bibi na jamaa wengine mashambani walikuwa salama. Wavyele wetu walimweleza kuhusu shughuli zao za kikazi nasi tukamjuza maendeleo yetu shuleni. Babu aliitikia kwa kutikisa kichwa na kutabasamu.

Baada ya muda, nilichukua simu nikaanza kuichezea. Dada naye alianza kutazama vipindi vya vibonzo kwenye runinga. Babu alimgeukia baba akamwambia, “Naona wajukuu wangu wamezama katika vyombo vya mawasiliano.” Baba aligeuka akatutazama bila kusema lolote. Babu naye alitua kidogo kisha akatuita karibu akaanza kusema nasi.

“Wajukuu wangu,” akasema, “Vifaa vya kidijitali ni muhimu sana maishani mwetu. Mwajua siku zetu tulingojea jamaa zetu watuletee habari za furaha au tanzia kutoka mbali. Hatukuweza kuyafahamu matukio ya kitaifa sembuse ya kimataifa. Watu wachache waliofika mjini kununua pembejeo za kilimo ndio waliotuletea habari ambazo aghalabu zilitiwa chumvi kupindukia. Redio zilimilikiwa na wachache sana.

Nyinyi mna bahati sana. Mnanunua simu za kisasa, tabuleti, viyuweo, tarakilishi na huduma za mtandao. Takriban kila nyumba ina redio na runinga. Mawasiliano kwenu ni rahisi sana. Mnaweza kupigiana simu, kuandikiana baruapepe au arafa. Hakika, ulimwengu umekuwa kama kijiji kidogo tu siku hizi. Hata matukio ya ughaibuni mnayatazama mbashara kwenye runinga zenu. Ibra iliyoje? Hakika manufaa ya vifaa vya kidijitali hayana kifani mkivitumia ipasavyo. Mtajiondolea upweke kwani mnaweza kuwajulia hali jamaa na marafiki kila uchao.”

Alitua kidogo tukadhani amehitimisha usemi wake kisha akaendelea, “Tafadhalini, nawaomba muwe waangalifu sana mnapovitumia vifaa hivi vya kidijitali. Hakuna masika yasiyokuwa na mbu. Kuna madhara chungu nzima ambayo yameibuka kutokana na matumizi ya vifaa hivyo. Tazameni yale mliyokuwa mkifanya muda mfupi tu uliopita. Kila mmoja alikuwa amezamia matumizi ya chombo chake mwenyewe. Nawaomba msikubali vyombo hivi vivuruge mshikamano wenu kama familia.” Hapo tuliinamisha nyuso zetu kwa aibu kisha babu akaendelea.

“Siku hizi habari za kupotosha zimeenea kama moto nyikani msimu wa kiangazi. Kuna matapeli wanaotumia simu kuwalaghai watu ili kuwaibia fulusi zao. Wengine wao wanaeneza uvumi mtandaoni na kuchochea vurugu katika jamii. Nawaomba msikubali kutumiwa na ibilisi kutenda mambo ya aina hiyo. Mnasikia wanangu na wajukuu wangu? Aidha, mwelewe kuwa ngoma ikivuma sana hupasuka kiwambo. Vifaa hivi vya kidijitali visichukue muda wenu wa kuwa pamoja.”

Babu alipohitimisha kauli yake, sote tuliafikiana naye huku kila mmoja akijisuta kimoyomoyo.

9. Yafuatayo ni madhara ya vifaa vya kidijitali kwa mujibu wa kifungu isipokuwa

  1. Akuwapotosha wanajamii
  2. Bkufanikisha mawasiliano
  3. Ckuvuruga mshikamano
  4. Dkutekeleza uhalifu.

Answer

B. kufanikisha mawasiliano

Kufanikisha mawasiliano ni manufaa, si madhara. Habari za kupotosha, kuvuruga mshikamano wa familia na utapeli ni madhara.

Answer this test freeGet it marked: create a free account

More Grade 8 Kiswahili questions from this test